KATIBA YETU

hp=3720010mwanzo Go to page 1 vile Madaraka ya Bunge, Uraia na kodi, lakini utekelezaji wake ulishindikana kupitia Taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu jitihada za kuondoa mambo ambayo ni vikwazo katika kutekeleza shughuli za Muungano ( Taarifa ya Kamati ya Shelukindo. Hata hivyo miaka kadhaa baadae Ripoti ya Shelukindo imeshindwa kutekelezwa kwa ukamilifu wake na kubakisha hali ya mivutano na mizozano ndani ya Muungano, kama ambavyo imekuwa kwa Tume nyengine nyingi ambapo inaonekana zaidi mtizamo wa Tume hizo ni kuiridhisha zaidi Zanzibar ibakie ndani ya Muungano kuliko kutafuta suluhu ya kudumu ya kero za Muungano na kuwa na maslahi kwa pande zote mbili za Muungano. Hali inakuwa ngumu zaidi kwa sababu baadhi ya mabadiliko yatahitaji kura ya maoni kwa upande wa Zanzibar. Na hata kama ingewezekana kuyarudisha kwenye Mamlaka ya Muungano, matatizo na kero za Muungano zisingemalizika bali zingeongezeka. Njia ya pili ni kuyakubali mabadiliko yaliyofanywa na kuongeza mengine ambayo yataipa Zanzibar uhuru wa kuamua (Autonomy) mambo yake ya uchumi. Hili linawezekana lakini likitokea ni lazima Tanganyika nayo ipate uhuru wa kuamua (Autonomy). Kwa maana hiyo kutakuwa na Serikali tatu na Serikali ya Muungano itabaki na mambo ambayo itakuwa na madaraka nayo kamili. Kutokana na malalamiko yanayotolewa na wananchi wa pande zote mbili ambayo Serikali zote mbili zimeshindwa kuyapatia ufumbuzi wa kudumu kwa muda mrefu, baadhi ya wananchi wa Zanzibar wanauona Muungano kuwa ni kero na baadhi ya wananchi wa Tanzania Bara wanauona Muungano kuwa ni mzigo. Aidha, wananchi wa Tanzania kwa kutumia Tume mbalimbali zilizoundwa kwa mfano Tume ya Nyalali na Kamati ya Kisanga walipendekeza Muungano wa Serikali tatu. Maoni hayo ya wananchi yamependekezwa tena mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na maoni hayo, Tume pia, ilipitia taarifa mbalimbali za utafiti na uzoefu wa nchi nyingine zenye changamoto za muungano. Katika kutoa mapendekezo hayo yenye lengo madhubuti la kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ilizingatia ya wananchi yanayoakisi matakwa na matarajio yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Tume nayo ilifanya utafiti na kuandaa ripoti juu ya Muungano inayopatikana katika ripoti za utafiti kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tatizo la msingi kabisa kwa Muungano wa Tanzania ni la muundo wenyewe wa Muungano wa Serikali mbili badala ya tatu ambao umetoholewa kutoka mifano ya miungano ambayo imeundwa kutokana na chimbuko la ukoloni kama ilivyokuwa kwa Page 67 54 United Kingdom of Great Britain na Northern Ireland pengine kwa sababu Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika wakati huo alikuwa ni Rolland Brown ambaye ni Mwingereza. Hali kadhalika, Muungano kama huo ulindwa Shirikisho la Malaysia ambalo lilijumuisha nchi ya Singapore ambayo baada ya muda mfupi ilijitoa. Takwimu za Tume zimeonyesha kwamba kwa upande wa Tanzania Bara, 13% walipendelea Serikali moja, 24% walipendekeza Serikali mbili na 61% walipendekeza Serikali tatu. Kwa upande wa Zanzibar, 34% walipendekeza Serikali mbili na 60% walipendekeza Muungano wa mkataba na 0.1% (watu 25) walipendekeza Serikali moja. Aidha, taasisi nyingi kama vyama vya siasa kwa mfano Chadema, CUF, NCCR Mageuzi;asasi za kiraia kwa mfano Legal and Human Rights Centre; - jumuiya za kidini kama Baraza la Maaskofu Tanzania, BAKWATA, Pentecost Council of Tanzania, Christian Professionals of Tanzania, Shuraa ya Maimamu, Baraza la Maimamu Zanzibar; , jumuia za wanasheria kama Zanzibar Law Society na Tanganyika Law Society, Law Academics; jumuia za wasomi; jumuia za wafanyakazi Zanzibar Trade Union ZATU, na Tanzania Union TUCTA, zilipendekeza muundo wa Serikali tatu. Baadhi ya taasisi za kiserikali ama moja kwa moja au kwa tafsiri ya mapendekezo yao, pia zilipendekeza serikali tatu. Kwa mfano, Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilipendekeza kuwepo kwa mamlaka huru ya Zanzibar, Mamlaka huru ya Tanganyika na Mamlaka ya Muungano na iwekwe wazi maeneo, uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya kila mamlaka; kwa upande wa Makatibu Wakuu wa Zanzibar hali kadhalika kwa tafsiri ya mapendekezo hayo pia yalijitokeza kama vile lilivyoona Baraza la Wawakilishi. Aidha, maoni yaliyotolewa na Ofisi ya Makamu Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zimependekeza mfumo wa Serikali tatu ili kuondoa kero za Muungano. Aidha, mamlaka ya Mapato Tanzania imependekeza kuwepo kwa Serikali tatu ili kutoa majibu ya kero zilizopo na kuleta utulivu zaidi ilimradi upangiliwe vizuri. Hivyo, muundo unaopendekezwa umezingatia kwamba: unaeleweka kwa urahisi katika ugawanyaji wa madaraka kati ya Mamlaka tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano kwa kila Mamlaka kuwa na Serikali yake; unawezesha nchi Washirika kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni, na hivyo, kuondoa hisia ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika ndani ya Muungano na Tanganyika kupoteza utambulisho na uwepo wake; unasaidia kila upande wa Muungano kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano kwa kadri inavyoona inafaa kwa maslahi ya maendeleo na ustawi wa watu katika eneo lake na hivyo kuondoa visingizio dhidi ya muungano; unaleta uwajibikaji kwa kila Serikali ya Nchi Mshirika na kuchochea kasi ya maendeleo na kukuza maslahi ya watu katika eneo husika na unapanua zaidi demokrasia kwa kupeleka madaraka kwa wananchi kujiamulia mambo yao. Rasimu hii inaweka vyombo na mfumo wa utatuzi wa mambo ya muungano na pia kuwepo na utaratibu wa kikatiba wa ushirikiano wa mambo yasio ya Muungano. Pia Rasimu inaweka dhahiri dhamana na majukumu na kujua nani mwenye dhamana gani Page 68 55 na mamlaka gani na kwa mipaka gani. Hivyo maamuzi yoyote yanaweza kuwa ya kutabirika na sio ya kushtukiza kama ilivyo hivi sasa na kuongeza tija na ufanisi jambo ambalo litaimarisha Muungano. Kwa mujibu wa maoni wananchi wengi waliopendekeza Muungano wa Serikali moja, walisema isipowezekana basi iwe ni Serikali tatu. Ibara ya 61: Vyombo vya Utendaji vya Jamhuri ya Muungano. a. Maudhui ya Ibara Ibara hii ya Rasimu ya Katiba inabainisha kuwepo kwa mihimili mikuu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama na majukumu na wajibu wa kila mhimili. Vyombo hivyo vinatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa kufuata masharti yaliyomo katika Katiba hii. b. Madhumuni na Lengo Kutambua kikatiba kuwepo kwa mihimili mitatu ya dola na mamlaka zao za kiutendaji ndani ya Jamhuri ya Muungano. Aidha, madhumuni mengine ni kutenganisha majukumu na mamlaka ya kila mhimili ili kuimarisha misingi ya udhibiti na urari wa madaraka (checks and balances). Lengo lingine ni kuviweka vyombo hivi chini ya Katiba kwa kufuata masharti yaliyomo ndani yake. c. Sababu ya Mapendekezo Dhana ya mgawanyo wa madaraka ni moja ya misingi muhimu ya kikatiba na ukatiba wa nchi inayoheshimu misingi ya demokrasia, utawala wa sheria na uwajibikaji wa serikali kwa raia. Hivyo, Ibara hii inaimarisha dhana hiyo ili kujenga taifa linaloongozwa kwa misingi ya uwajibikaji kwa wananchi na kuheshimu haki za binadamu. Vile vile kuifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imara kisiasa na yenye mfumo wa utawala unaoeleweka na kutabirika. Dhana hii imekuwepo katika katiba za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa wakati wa kipindi cha utawala wa chama kimoja (1965-1992) mihimili yote hii iliwekwa chini ya mamlaka ya chama tawala na kutekeleza maamuzi ya chama hata kama yalikuwa hayaendani na matakwa ya Katiba. Na baina ya mihimili mitatu hiyo ya dola, mhimili wa utendaji ulipewa mamlaka makubwa zaidi kuliko mihimili mengine miwili iliyobakia. Ibara ya 62: Mamlaka ya Serikali ya Muungano a. Maudhui ya Ibara Ibara hii ya Rasimu ya Katiba inaipa Serikali ya Jamhuri ya Muungano mamlaka kamili juu ya usimamizi na utekelezaji wa mambo yote ya Muungano iliyokabidhiwa chini ya Katiba hii. Ibara hii inatoa nafasi kwa Serikali ya Muungano kutekeleza mambo yasiyo ya Muungano itakayokabidhiwa na Nchi Mshirika kwa hiyari na makubaliano kwa masharti Page 69 56 maalum. Katika utekelezaji wa shughuli zake kwa Mambo ya Muungano au yasiyo ya muungano, Serikali ya Muungano italazimika kufuata masharti ya Katiba hii. b. Madhumuni na lengo Madhumuni ya Ibara hii ni kuweka misingi ya Kikatiba kwa Serikali ya Muungano katika kutekeleza Mambo ya Muungano. Pia kuweka fursa ya kikatiba kwa Nchi Washirika kuweza kukasimu mamlaka yake kutekelezwa na Serikali ya Muungano kwenye mambo yasiyo ya Muungano. Kuiwezesha Serikali ya Shirikisho kutekeleza majukumu yake kiufanisi katika Mambo ya Muungano. Vile vile ni kuweka msingi wa Serikali kutii Katiba katika utendaji na shughuli zake. c. Sababu za Mapendekezo Ibara hii imezingatia kuwa katika miundo ya muungano inayotenganisha mambo ya muungano na mambo yasiyo ya muungano, huyaweka mamlaka yote ya mambo ya muungano kwenye serikali ya muungano. Katika usimamizi na utekelezaji wake mamlaka hayo hayaruhusiwi kukasimiwa au kuingiliwa na mshirika yoyote wa muungano. Huo ndio ukuu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano na Serikali yake katika mamlaka ya Muungano. Sababu nyingine ni kuweka msingi kwa Jamhuri ya Muungano kusimamia kikamilifu wajibu wake katika Muungano. Kwa mara ya kwanza Rasimu hii inajenga msingi wa ushirikiano (cooperation), mshikamano (solidarity) na kufikia kina cha ufanisi (subsidiarity) kwa kuweka kipengele cha Nchi Mshirika kuwa na fursa ya kuiomba Serikali ya Muungano kutekeleza mamlaka yaliyo chini yake kuweza kufikia malengo na matakwa yake kwa manufaa na ustawi wa wananchi. Dhana hii inasaidia zaidi kujenga muungano kwa vile inaweka mkazo kwa Serikali Jamhuri ya Muungano kutafuta kila njia kufanya kazi na Serikali za Nchi Washirika, na pia Serikali za Nchi Washirika kuwa karibu zaidi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Pia kujenga na kudumisha utamaduni wa Nchi Washirika kuweza kushirikiana baina yao. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba mamlaka ya Serikali ya Tanganyika au Serikali ya Zanzibar ni kwa mambo yasiyo ya Muungano tu na siyo vinginevyo. Ibara ya 63: Mambo ya Muungano a. Maudhui ya Ibara Ibara hii ya Rasimu ya Katiba ikisomwa pamoja na Nyongeza ya Katiba inaainisha mambo saba (7) ya Muungano kama ifuatavyo: 1. Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2. Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 3. Uraia na Uhamiaji. Page 70 57 4. Sarafu na Benki Kuu. 5. Mambo ya Nje. 6. Usajili wa Vyama vya Siasa. 7. Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya Kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano. b. Madhumuni na Lengo Lengo la Ibara hii ni kuainisha na kutofautisha Mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya muungano ili kuleta ufanisi wa utekelezaji. Kwa kupunguza mambo ya Muungano kunaondoa kero zilizotokana na kuongezeka kwa Mambo mengi ya Muungano. Kurudi kwenye mambo ya msingi ya muungano yenye sifa ya kutambulisha mamlaka ya dola (Sovereign Functions) na kwenye dhana ya asili ya Waasisi wa Muungano kama yalivyoainishwa kwenye Hati ya Muungano ya 1964. Muhimu zaidi ni kuweka mipaka ya kikatiba kwa mamlaka ya muungano ambayo hayastahiki kuchezewa au kuingiliwa kuepukana na uvunjifu wa katiba. c. Sababu za Mapendekezo Kwa mujibu wa Ibara hii ya Rasimu ya Katiba, Mambo ya Muungano yaliyopendekezwa ni saba badala ya 22 yaliyoorodheshwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Mambo mengine yaliyozingatiwa katika Rasimu hii ni kuhakikisha mambo makuu ya kidola (Sovereign Functions) yanabaki chini ya Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano. Mambo hayo ndiyo yanayoitambulisha nchi katika medani za sheria na mahusiano ya kimataifa na ndani ya nchi hayana budi yawe ya Muungano. Rasimu hii imezingatia mambo 11 ya awali yaliyokuwemo katika Hati ya Makubaliano ya Muungano na Katiba ya awali ya Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, masuala ya Bandari na Usafiri wa Anga ambayo ni Mambo ya awali ya Muungano yameachwa katika orodha mpya ya Mambo ya Muungano kwa sababu hayajawahi kutekelezwa kimuungano kwa makubaliano ya Serikali mbili. Mambo mengine ya Muungano yaliyoachwa ni yale 11 yaliyoongezwa baadaye ambayo ndio yamekuwa chanzo cha malalamiko na kero za Muungano. Kigezo kilichotumika katika kuamua Mambo ya Muungano katika Rasimu hii ni pamoja na kuhalalisha makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au kwa hatua zilizochukuliwa na upande mmoja wa Muungano kutekeleza au kutokutekeleza Mambo ya Muungano bila ya kubadilisha Katiba. Mapendekezo haya yanakidhi haja ya wananchi walio wengi waliotoa maoni yao ya kutaka kuondoa kero za Muungano ambazo kwa kiasi kikubwa zimetokana na muundo wa Serikali mbili kwa kukosekana kwa mipaka iliyo wazi baina ya Mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya muungano. Jumla ya maoni 2,452 yalitolewa katika pande zote mbili za Muungano juu ya Orodha ya Mambo ya Muungano. Maoni 6 katika kila 10 (61.9 asilimia) yalitaka mambo ya Muungano yapunguzwe hasa kutoka Tanzania Zanzibar. Waliotaka mambo yapunguzwe kutoka Tanzania Zanzibar ni asilimia 79.3 na kutoka Tanzania Bara ni asilimia 44. Page 71 58 Rasimu inapendekeza katika hali mpya ya kuwa na mambo machache ya Muungano ambayo yataweka mipaka baina ya Serikali zote tatu Ibara ya 64: Nchi Washirika a. Maudhui ya Ibara Ibara hii ya Rasimu ya Katiba inatambua kikatiba Nchi Washirika wa Muungano kuwa ni Tanganyika na Zanzibar. Pia inaweka mamlaka zao za utekelezaji kwa mambo yasiyo ya Muungano yanayohusu Nchi Washirika katika serikali zao kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba zao